Hii ndio Sababu ya wagonjwa kuacha kutumia ARVs.

2:47:00 PM

LUGHA chafu, unyanyapaa na kutoa siri za wagonjwa vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa vituo vya afya, vimetajwa kuchangia wananchi kutojitokeza kupima afya, huku wagonjwa wa Ukimwi  wakiacha kutumia dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi (ARVs).

Hayo yalielezwa jana na Mwenyekiti wa Taifa wa Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (NACOPHA), Justine Mwinuka, wakati wa uzinduzi wa mpango mkakati wanne wa VVU na Ukimwi katika sekta ya afya na sherehe za miaka 30 ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi.

Mwinuka alisema vitendo vya kutoa siri za wagonjwa, lugha chafu na unyanyapaa vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa afya ni miongoni mwa mambo yanayochangia watu wengi kushindwa kufika kwenye vituo hivyo kupima afya zao na wengine kuacha  kutumia dawa.

“Mheshimiwa Waziri, changamoto hizi na nyingine huzorotesha upatikanaji wa matokeo yaliyotarajiwa ya matibabu ya kufubaza virusi, kwa kuwa huchangia watu kutokwenda vituoni kabisa au kuacha matibabu,” alisema Mwinuka.

Alisema lugha za kejeli za kuwabeza wagonjwa wanaofika kupata huduma, dawa za kufubaza virusi zimechangia kwa wagonjwa kutoendelea kufika vituo hivyo  kupata matibabu hasa kundi la vijana.

Mwinuka alitaja changamoto zingine ni upatikanaji wa dawa za magonjwa nyemelezi na kuiomba serikali kusaidia upatikanaji wa dawa hizo, kuboreshwa zaidi pamoja na kutumia muda mwingi kwenye vituo hivyo kusubiri matibabu.

Changamoto zingine ni umbali wa vituo vya kutolea ARVs hasa maeneo ya vijijini, wagonjwa kuachwa vituoni bila kupewa huduma na kuzuiliwa kuchukulia dawa.

Akizindua mpango huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema hajaridhishwa na takwimu za kupungua kwa maambukizi hayo nchini.

Mwalimu alisema kwa muda wa miaka mitano takwimu zinaonyesha maambukizi hayo yamepungua kwa asilimia 0.4 kutoka asilimia 5.1 hadi 4.7, kiasi ambacho ni kidogo sana.

Aidha, alisema wakati takwimu zikionyesha kuwa maambukizi ya kitaifa yanapungua, lakini takwimu za baadhi ya mikoa zinaonyesha kupanda zaidi kwa maambukizi ya ugonjwa huo.

Alitaja sababu zilizosababisha maambukizi kuongezeka ni kupungua kwa nguvu ya kampeni ya maambukizi katika mikoa iliyokuwa na idadi ndogo ya wagonjwa wa Ukimwi.

Naye, Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kupambana na Ukimwi, Dk. Angela Ramadhani, alisema malengo ya mkakati wa nne wa mapambano dhidi ya Ukimwi yanalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwahamasha walioambukizwa kutumia ARVs, ili kuzuia maambukizi zaidi. 

Related Posts

Previous
Next Post »